SIKU chache baada ya serikali kusitisha Opereshini Tokomeza
Ujangili kutokana na wabunge kuilalamikia wakidai inakiuka haki za
binadamu na mifugo mingi imeuawa, siri imefichuka kwamba baadhi ya
wabunge na vingozi wa serikali wanatumiwa na majangili kudhoofisha vita
dhidi ya ujangili.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kutoka bungeni na serikalini, majangili
hao wamegawanyika katika makundi sita. Wamo wafugaji, wakulima,
watalii, wamiliki wa vitalu vya uwindaji, wabunge, na viongozi wa
serikali ambao wameibuka na kuingilia kati baada ya kuhisi kwamba
wanakaribia kukamatwa.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa zaidi ya sh milioni 200 zimechangwa
na majangili hao kwa ajili ya kufanikisha mkakati wa kuzima opereshini
hiyo.
Baadhi ya wabunge wanatumiwa bila kujua, huku wengine wakifanya hivyo kwa hiari na makusudi ya kunusuru majangili.
Tayari kuna mpasuko mkubwa serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kutokana na baadhi ya watendaji kubaini mbinu chafu za kutaka
kuzima operesheni hiyo ili kuwanufaisha vinara wa ujangili.
“Hawa watu wana mtandao mkubwa, baada ya kubaini wanakaribia kunaswa,
sasa wameingia bungeni kwa kuwatumia baadhi ya wabunge ili waipinge
operesheni hiyo,” kilisema chanzo.
Taarifa za uhakika kutoka serikalini zinasema kuwa majangili hao
wamekuwa na jeuri kutokana na kuwazunguka viongozi wa chini na
kuwasiliana moja kwa moja na kigogo, ambaye bila kujua amekuwa
akizunguka viongozi wa wizara, na kukingia kifua majangili.
Baadhi ya vyanzo hivyo vilieleza kushangazwa na hatua ya baadhi ya
wabunge kutetea uhai wa ng’ombe na kushindwa kulinda uhai wa tembo
wanaouawa na kung’olewa pembe.
Mwishoni mwa wiki, Bunge liliazimia kuunda kamati teule ili
kuchunguza suala hilo huku Waziri Mkuu na mawaziri wanne wakisulubiwa
kwa madai kuwa wameshindwa kuwajibika ipasavyo.
Mbali na Pinda, wamo pia Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani),
Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo na
Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Hata hivyo, gazeti hili limedokezwa kuwa kwa vyovyote iwavyo serikali
haitakuwa tayari kukubali kamati teule hiyo iundwe kwani ripoti yake
inaweza kumng’oa Pinda na hivyo serikali kuanguka.
“Kinachofanyika sasa ni kuletwa kwa taarifa ya dharura bungeni ya
kuonyesha serikali inapendekeza njia mbadala ya kushughulikia suala
hilo ili badala ya kamati teule, iundwe tume huru itakayoongozwa na jaji
kama ambayo CHADEMA wamekuwa wakipendekeza muda mrefu.
“Vita hii ya ujangili ni pana, imeingia hadi kwenye siasa za makundi
ya urais ndani ya CCM, na hivyo kundi moja linataka kumng’oa Makinda
kwenye uspika kwa hofu kuwa anawasikiliza sana wabunge na mawaziri wa
kundi jingine,” kilisema chanzo hicho.
Kwamba Oparesheni Tokomeza Ujangili inapingwa baada ya vinara hao
kubaini wanakaribia kunaswa, na sasa wanataka kuvuruga ili kazi hiyo
irudi nyuma na hata ikiendelea basi wako radhi kutajana kwa majina
kwani miongoni mwao wamo pia wabunge na viongozi wengine.
“Hawa majangili wana jeuri, wao wanazungumza kwa simu moja kwa moja
na mmoja wa vigogo wa ngazi za juu serikalini, na huko wanasikilizwa.
Serikali nayo inajua kuwa operesheni ikisimama tembo wanakwisha na vile
vile kamati teule wakiikubali serikali inaanguka,” kinasisitiza
chanzo.
Vyanzo hivyo vinaainisha kuwa hata mchakato wa kutaka kumwondoa
Makinda kwenye uspika ambao ulikuwa umeanza kupitia kwa Mbunge wa
Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla kukusanya kura za wabunge uliingiliwa na
majangili hao.
Vyanzo vya habari vinasema hoja ya Kigwangalla inasukumwa na wakubwa
kadhaa mashabiki wa mmoja wa mawaziri waandamizi wanaotajwa kutaka
kugombea urais 2015, ambao wanaona Makinda anapendelea wabunge
wanaoshabikia kambi ya kigogo mwingine anayesemekana kutaka urais kwa
udi na uvumba.
Habari zinasema kundi la waziri huyo linaungwa mkono na kigogo mmoja
mwandamizi ambaye hataki kabisa kuruhusu swahiba wake wa zamani agombee
urais; na sasa wamedhamiria kumwangusha Makinda.
Hata hivyo, kabla hoja yao haijashika kasi, wakati wakiendelea
kukusanya sahihi za kutosha kumwondoa Makinda, majangili nao wakapata
upenyo kwa kuathiri mwelekeo wa Bunge, na Makinda anaruhusu mjadala wa
ujangili, ambao iwapo kamati teule itaundwa na kufanya kazi yake
barabara, serikali inaweza kuangushwa kabla ya spika huyo kuondolewa.
“Hoja ya Makinda imezimwa, sasa wabunge wanazungumzia operesheni ya
ujangili. Hapa wanajua kuwa spika hawezi kukubali hoja hiyo iendelee,
hivyo naye ataipa kipaumbele kamati teule ili kuonyesha serikalini kuna
tatizo.
“Wanajua hawawezi kumfukuza spika katika kikao hiki, lakini wakati
huo Kamati ya Bunge itakuwa imekamilisha mchakato na kutoa uamuzi dhidi
ya Pinda na mawaziri wenzake, jambo ambalo linaweza kumnusuru Makinda
na kuiangusha serikali,” kilisema chanzo chetu.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), ndiye alitaka Bunge lijadili
kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, huku
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), akitaka Bunge lijadili vitendo
vinavyofanywa na watendaji katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Lugola alidai watendaji wamekuwa wakiwaua kwa risasi ng’ombe
waliowakamata kwenye operesheni hiyo pamoja na kuwatesa wamiliki
wasiotoa fedha zinazohitajika.
Kutokana na hoja hizo, Makinda alitoa fursa kwa Waziri wa Maliasili
na Utalii, Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Mathayo, kuelezea Operesheni Tokomeza Ujangili na migogoro kati ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Kagasheki ndiye aliyekuwa wa kwanza kueleza operesheni hiyo
inaendelea. Alisema inalenga kutokomeza ujangili ulioshamiri hapa
nchini kiasi cha kutishia sekta ya utalii na tembo.
Hata hivyo, Kagasheki alisema kutokana na malalamiko ya watu
mbalimbali juu ya mwenendo wa operesheni hiyo, serikali imeamua
kuisitisha ili kufanya tathmini.
Waziri huyo pia alisema mifugo yote iliyokamatwa ndani ya hifadhi
kabla na baada ya operesheni hiyo iachiliwe bila gharama yoyote na watu
wenye ushahidi wa ng’ombe wao waliouawa kwa risasi wawasilishe
vielelezo ili achukue hatua zaidi.
Waziri Mathayo alitoa taarifa kuhusu migogoro kati ya wafugaji na
wakulima. Aliwaomba radhi waliopata hasara ya kujeruhiwa, kupoteza
mifugo au vifo katika operesheni hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: